By :Amina Abdullahi
Naibu Rais Kithure Kindiki amesema kuwa serikali imejitolea kuhakikisha kuwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2027 utakuwa huru, wa haki na wa amani katika ngazi zote za uongozi nchini.
Amesisitiza kuwa serikali haitaruhusu machafuko ya kisiasa kabla au baada ya uchaguzi, akieleza kuwa ni wajibu wa kila Mkenya kulinda amani na mshikamano wa taifa.
Akizungumza katika hafla ya kuwawezesha kiuchumi wafanyabiashara wadogo kupitia vyama vya ushirika (SACCOs) katika Eneo Bunge la Gatundu Kusini, Kindiki amesema serikali ya Kenya Kwanza inaendelea kutekeleza mabadiliko ya kiuchumi kutoka ngazi ya chini kwenda juu (bottom-up), kama ilivyoainishwa katika ilani ya serikali.
“Uchaguzi wa 2027 uakuwa wa Huru na hakuna m yoyote tutaruhusu apiganishe wakenya,” Kindiki alieleza.
Ameeleza kuwa mojawapo ya mikakati hiyo ni kuwainua wafanyabiashara wadogo kwa kuanzisha zaidi ya masoko 400 ya kisasa katika maeneo mbalimbali nchini, pamoja na kuboresha miundombinu ya kibiashara ikiwemo vituo vya kuhifadhi bidhaa kwa baridi, vibanda vya kisasa vya biashara na vituo vya TEHAMA ili kukuza ujasiriamali wa kidijitali.
Aidha, serikali imezindua Mpango wa Nyota wa thamani ya Shilingi bilioni 28 unaolenga kusaidia biashara ndogo na za kati (MSMEs) katika wadi zote 1,450 nchini. Kupitia mpango huu, biashara angalau 70 katika kila wadi zitapokea mtaji wa Shilingi 50,000 kila moja ili kusaidia uundaji wa ajira na kuongeza kipato kwa wananchi katika maeneo ya mashinani.
Wabunge waliohudhuria hafla hiyo ni pamoja na GG Kagombe (Gatundu Kusini), Ann Muratha (Mwakilishi wa Wanawake, Kiambu), Elijah Njoroge Kururia (Gatundu Kaskazini), Alice Ng’ang’a (Thika Town), Machua Waithaka (Mji wa Kiambu), Mburu Kahangara (Lari), Simon King’ara (Ruiru).
Wengine ni James Githua Wamacukuru (Kabete), John Njuguna Kawanjiku (Kiambaa), Veronica Maina (Seneta Mteule), Florence Jematiah (Mwakilishi wa Wanawake, Baringo), Kuria Kimani (Molo), na Geoffrey Mulanya (Nambale), pamoja na Wajumbe wa Bunge la Kaunti (MCAs).